Kuzuka upya kwa mapigano mashariki mwa Ukraine hivi karibuni kumesababisha watu 28 kupoteza maisha yao na kuzusha hofu kwamba kupamba moto huko kwa mapigano kutavuruga makubaliano ya kusitisha mapigano yaliopatikana kwa taabu chini ya usimamizi wa Ufaransa na Ujerumani kwa miezi minne.
Obama bila ya kuitaja kwa jina Ugiriki iliokumbwa na mzozo wa kiuchumi pia amegusia matatizo yanayoendelea kuwepo kati ya Umoja wa Ulaya na Ugiriki ilioelemewa na mzigo wa madeni kwa kutaja kwamba mada za juu katika mkutano huo wa kilele ni uchumi wa dunia ambao unazalisha ajira na kuleta fursa na kuendelea kuufanya Umoja wa Ulaya uwe madhubuti na wenye neema.
Merkel anayatetea mageuzi magumu na kubana matumizi ili Ugiriki iweze kupatiwa mikopo amefanya juhudi za mwisho kuupatia ufumbuzi mzozo huo wa Ugiriki siku chache kabla ya mkutano huu wa Kundi la Mataifa Saba ambapo amekuwa na mashauriano na viongozi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya mjini Berlin.
Suala la Ugiriki linatishia kuugubika mkutano huo wa kilele ambao Merkel alitaraji kulenga kwenye matatizo mengine makuu kuanzia na mabadliko ya tabia nchi na Waislamu wa itikadi kali, haki za wanawake, miradi ya afya kwa wananchi na vita dhidi ya umaskini.
Siku moja baada ya kunadamana dhidi ya kundi hilo la G7 katika maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani waandamanaji kadhaa Jumapili walikuwa wamezinga njia kuelekea kwenye kasri ya ngome ya Elmau unakofanyika mkutano huo jambo ambalo limepelekea waandishi kupelekwa kwa helikopta kwenye eneo la mkutano huo.